Jumatano, 27 Julai 2022

DKT. AGNES KIJAZI AKABIDHIWA UFUNGUO WA JIJI LA ENTERPRISE, ALABAMA-MAREKANI


Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani Bw. William E. Cooper, akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi, ufunguo wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani







Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani Bw. William E. Cooper, akitoa maelezo kuhusiana na Funguo ya Jiji la Enterprise-Alabama, Marekani na Sanamu ya Kumbukumbu ya Historia ya Jiji hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi na Mjumbe wa Bodi ya TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Miundombinu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka.



Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani Bw. William E. Cooper, akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi, Sanamu ya kumbukumbu ya historia ya Jiji la Enterprise


Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi akiongozana na Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani wakati wa zoezi la uhakiki wa utendaji kazi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa Songwe na Kigoma.


Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi akiteta jambo na Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani wakati Mtahiki Meya huyo alipowatembelea wataalamu wa TMA wakati wa zoezi la uhakiki wa utendaji kazi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa Songwe na Kigoma.


Mstahiki Meya wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani Bw. William E. Cooper, (wa pili kutoka kushoto) katika picha eneo la majaribio ya utendaji wa Rada na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi, Mjumbe wa Bodi ya TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa ‘transport’ wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka (wa kwanza kutoka kushoto) na Meneja Mradi wa EEC, Bw. Patrick Lamar (wa kwanza kulia) anayeratibu zoezi la uhakiki wa utendaji kazi wa Rada za hali ya hewa zitakazofungwa Songwe na Kigoma


Ufunguo wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani uliokabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi

Ufunguo na Samamu ya kumbukumbu ya historia vya Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani alivyokabidhiwa Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt Agnes Kijazi ikiwa ni heshima ya kumkaribisha katika Jiji hilo kama mkazi.

Enterprise, Alabama, Marekani, 26 Julai 2022

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi, amekabidhiwa ufunguo wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani na Mstahiki Meya wa Jiji hilo Bw. William E. Cooper alipowatembelea wataalamu kutoka TMA na mjumbe kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) wanaoshiriki katika zoezi la kuhakiki utendaji kazi wa radar za hali ya hewa (“Factory Acceptance Test (FAT)”) katika kiwanda cha Enterprise Electronics Corporation-EEC kilichopo katika Jiji la Enterprise, kuanzia tarehe 18 hadi 29 Julai, 2022. 

 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mstahiki Meya Cooper alisema amefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya EEC na TMA katika eneo la ununuzi na matengenezo ya Rada za Hali ya Hewa, na kuwakaribisha katika mji wa Enterprise. Kwa heshima ya ushirikiano huo, Mstahiki Meya alimkabidhi Dkt Kijazi Ufunguo wa Jiji la Enterprise ikiwa ni heshima ya pekee kuwa anakaribishwa  katika Jiji la Enterprise.

 

“Nakukabidhi ufunguo huu kama alama ya heshima unayopewa katika jiji la Enterprise kwamba unaweza kuingia na kutoka upendavyo, aidha, umjulishe Balozi wa Marekani nchini Tanzania kuhusu wewe kupatiwa ufunguo huu”. Alisema Bw. Cooper.

 

Aidha, Mstahiki Meya pia alimpatia zawadi ya sanamu ya kumbukumbu ya historia ya Jiji la Enterprise yenye kuelezea namna mdudu mharibifu wa zao la pamba (boll weevil) alivyobadilisha shughuli za kilimo za eneo la Enterprise kutoka kilimo cha zao la pamba miaka ya 1800 hadi 1900 na kugeukia kilimo cha zao la karanga ambalo limekuwa na manufaa makubwa katika uchumi wa jiji la Enterprise. 

 

“Mabadiliko hayo yamefanya mdudu huyu aheshimiwe kwamba kupitia uharibifu wake amesababisha mageuzi yenye mafanikio katika sekta ya kilimo.Ukipita katika baadhi ya maeneo ya jiji hili la Enterprise utaona sanamu hii ambayo ina historia muhimu katika mageuzi ya kilimo katika jiji hili”. Alieleza Bw. Cooper.

 

Kwa upande wake, Dkt. Kijazi alimshukuru Mstahiki Meya Cooper kwa kutenga muda wake na kuja kuwasalimia wakati wa zoezi hilo la ukaguzi wa matengenezo ya mitambo miwili ya Rada za hali ya Hewa zitakazofungwa mkoani Songwe na Kigoma, Rada ambazo zimegharamiwa na Serikali ya Tanzania.



 

Alhamisi, 23 Desemba 2021

WATAALAMU WATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA.

Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara (MB) akizungumza kabla ya kukizindua rasmi kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021.  



Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi akitoa neno la ukaribisho kwa mgeni rasmi kabla ya uzinduzi wa kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021. 


Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), akifafanua jambo kabla ya uzinduzi rasmi wa kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021. 


Mwandishi wa kitabu hicho, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Huduma za Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang'a akielezea chimbuko la kuhamasika kuandika kitabu hicho cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021.  


Mgeni Rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania baada ya kuzinduliwa rasmi kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021.


Mgeni Rasmi akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) baada  ya kuzinduliwa rasmi kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, Katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza, Tarehe 23/12/2021. 



Dar es Salaam; Tarehe 23 Disemba, 2021;

Wataalamu nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye tija na kuelimisha jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuandika vitabu. Hayo yalizungumzwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara (MB) wakati akizindua rasmi kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza,Tarehe 23/12/2021. 

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii na kuwaandaa na kuwataka wataalamu kutoa mchango chanya wa kusaidia kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya tafiti na kuelimisha jamii”. Alizungumza Mhe. Waitara.

Aidha, Mhe. Naibu Waziri alitoa wito kwa umma kukitumia vizuri kitabu hicho ili kujipatia elimu na uelewa zaidi kuhusiana na changamoto za hali ya hewa hapa Tanzania katika kupanga na kutekeleza mipango ya kijamii na kiuchumi kwa tija na ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waitara aliipongeza Bodi na Menejimenti ya TMA kwa usimamizi na kazi kubwa ya kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwemo utabiri mzuri uliotolewa wa kuhusiana na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi kwa msimu huu wa mvua.

“Maeneo mengi yamekuwa na upungufu mkubwa wa mvua kama ambavyo mlisema katika taarifa yenu ya mwezi Septemba,2021. Utabiri na tahadhari mnazozitoa zinamchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii na pia katika utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati kama ya SGR na Ujenzi wa Bwawa la Nyerere”. Alifafanua Mhe. Waitara.

Awali wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alisema Kitabu hicho ni cha sayansi ya hali ya hewa kinachoweza kutumika kwa ajili ya kuendeleza tafiti za hali ya hewa hasa kwa Tanzania na suala la kujivunia ni kuwa kitabu hicho kimeandikwa na mmoja wa wataalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambaye ni Dkt. Ladislaus Chang’a.

 Akizungumzia mafanikio ya kitabu hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alifafanua kuwa kitabu hiki kinatoa mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa changamoto za hali ya hewa kwa watu wote hususan wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu pamoja na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma, watafiti, makandarasi na watunga sera. 

“Baadhi ya maudhui ambayo yamewekwa katika kitabu hiki ni pamoja na tathmini ya hali ya klimatolojia na mwelekeo wa joto, mvua, unyenyevu na upepo, ambapo uelewa wake ni wa muhimu sana kwasasa na hata kwa wakati ujao ili kupanga na kutekeleza shughuli zote za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo, Nishati, Afya, Maji na Usafiri”. Alifafanua Dkt. Kijazi.

Naye, mwandishi wa kitabu hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Huduma za Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza chimbuko la kuhamasika kuandika kitabu hicho ni kutokuwepo kwa kitabu cha namna hiyo katika kufundisha kozi za klimatolojia na mabadiliko ya hali ya hewa UDSM na SUA, ushiriki mdogo wa wanasayansi wa Afrika katika masuala ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa katika Jopo la Kiserikali la Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani – IPCChamasa na msukumo mdogo katika masuala ya sayansi na utafiti miongoni mwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa Tanzania na Duniani.

Jumatatu, 31 Mei 2021

KIPUPWE 2021: VIPINDI VYA UPEPO MKALI WA KUSI VINATARAJIWA KATIKA MAENEO MENGI YA NCHI.



 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa kwa Tanzania kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2021, taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumzia msimu huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi kufuatilia utabiri huo wa msimu wa Juni-Agosti (JJA) 2021, hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali wa Kusi vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.

Kwa kawaida msimu wa kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi, kutokana na matarajio ya uimarikaji wa wastani wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa Afrika vipindi vichache vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokezaHata hivyo,katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi”. Alisema Dkt. Kijazi.

Akizungumzia hali ya baridi hususan maeneo yenye miinuko, Dkt. Kijazi alisema, Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hususan nyakati za usiku na asubuhi na vipindi vya baridi kali zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai 2021. 

“Hali ya baridi inayotarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 6 hususan maeneo yenye miinuko katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro, hivyo, inaweza kuleta athari kwa binadamu, wanyama, samaki pamoja na ustawi wa mazao mashambani hususani mazao ya muda mrefu kama migomba yanaweza kupata magonjwa ya fangasi na kudhoofisha ustawi wake. Hali hii imesababishwa na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu linatarajiwa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.

 

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa, kwa ujumla hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya kawaida katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, maeneo ya Ukanda wa Pwani (Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Nyanda za juu kaskazini mashariki (Kilimanjaro, Arusha na Manyara), ukanda wa Ziwa Victoria na magharibi mwa nchi (Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma), hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya juu kidogo ya kiwango cha kawaida. Kwa upande wa maeneo ya kanda ya kati (Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini magharibi(Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe)na mkoa wa Ruvuma hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa chini kidogo ya joto la kawaida kama ilivyozoeleka.

 

Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo wa Matlaivinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara). Aidha, katika ukanda wa Ziwa Victoria vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache. 

 

Kwa upande wa athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema, Hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na  kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.

 

Kwa taarifa zaidi tembelea; www.meteo.go.tz

http://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast




Jumamosi, 16 Januari 2021

TMA YAENDELEA KUMILIKI CHETI CHA UBORA WA HUDUMA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA KWA KIPINDI CHA MIAKA KUMI (10) SASA.


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kumiliki cheti cha kimataifa cha uthibitisho wa utoaji huduma bora za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga kwa mara nyingine. Mamlaka ambayo imekuwa na cheti hiki kwa miaka kumi sasa, ni miongoni mwa Taasisi chache za hali ya hewa barani Afrika kufanikiwa kushikilia cheti hicho kwa kipindi kirefu.

Mafanikio hayo yamepatikana  baada ya kukamilika kwa ukaguzi uliofanyika kwa njia ya mtandao na Kampuni ya Kimataifa ya Certech kutoka Canada, kuanzia Tarehe 11 hadi 15 Januari 2021 katika vitengo na ofisi mbalimbali ndani ya Mamlaka, Makao Makuu na Mikoani. Ukaguzi huu ulifanyika kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO 9001:2015) na ulimalizika kwa taarifa nzuri ya kwamba TMA imeboresha sana mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo inastahili kuendelea kumiliki cheti hicho cha ubora cha kimataifa. 

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alisema kuwa Mamlaka imeanza kumiliki cheti hicho cha ubora tangu mwaka 2011, ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho kwa vigezo vya ubora vilivyoainishwa katika mwongozo wa “ISO 9001:2008”, na ilipofika mwaka 2017 Tanzania kupitia TMA ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha inafanikiwa kupata cheti kipya kwa mujibu wa vigezo vipya vya “ISO 9001:2015,” ambacho kiliifanya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa nchi ya tatu barani Afrika ambayo taasisi yake ya hali ya hewa imepata cheti hicho kabla ya Septemba 2018  iliyokuwa ni mwisho wa matumizi ya cheti cha zamani.

“Mamlaka imekuwa ikikaguliwa kimataifa kila mwaka na mkaguzi kutoka nje ya nchi ili kuangalia ubora wa huduma zitolewazo, ni furaha kubwa kuona bado TMA inaendelea kuwa taasisi ya mfano kwa taasisi zingine za hali ya hewa barani Afrika na nje ya Afrika kwa kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa. Mpaka sasa TMA imefanikiwa kutoa mafunzo kwa baadhi ya taasisi za hali ya hewa katika nchi  za SADC, EAC na zingine zikiwemo Saudi Arabia, Libya, Nigeria, Maldives, n.k kuhusu jinsi ya kufanikisha upatikanaji wa cheti hiki pamoja na kuboresha weledi wa wataalamu katika Taasisi zao za Hali ya Hewa. Mafanikio haya ni kutokana na ‘team work’ iliyopo baina ya menejimenti na watumishi wa Mamlaka, weledi, bidii na miongozo mizuri tuliyojiwekea ya kuhakikisha tunafanikiwa ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa ukaguzi wa ndani mara kwa mara”. Alisema Dkt. Kijazi.

Aliongeza kwa kusema kwamba upatikanaji wa cheti hicho unaihakikishia dunia kwamba anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa liko salama kwa ndege zote za kimataifa kuruka kwani ilishakubalika kimataifa kwamba kwa nchi ambazo taasisi zao za hali ya hewa hazijapata cheti hicho cha ubora ndege hazitaruka katika anga la nchi hizo. Dkt. Kijazi alisema TMA inajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia sekta ya usafiri wa anga kwani katika viwanja vyote vya ndege nchini huduma za hali ya hewa zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Hata katika viwanja ambavyo ndege hazitui kwa saa 24, TMA inaendelea kupima hali ya hewa katika viwanja hivyo kwa saa 24 ili kukidhi matakwa ya kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Aliwapongeza watumishi wa TMA kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha TMA inatimiza majukumu yake.

Awali wakati akikamilisha ukaguzi huo, mkaguzi wa nje kutoka Certech - Canada Bwana Frank Strohmeier, alisema TMA imekuwa ikiboresha kila mara mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo kwa mwaka huu, hapakuwa na hoja (nonconformity) yoyote ambayo ingehitaji kutolewa maelezo na kupelekea kuhitajika kwa marekebisho katika mfumo wa utoaji huduma. Hivyo maeneo yote ambayo TMA imekaguliwa yamekuwa na ubora wa hali ya juu pasipo kuwa na mapungufu yoyote. Alifurahishwa na jinsi ambavyo ukaguzi umefanyika kwa njia ya mtandao ukiwa na mafanikio makubwa pasipo changamoto yoyote ya teknolojia hivyo akawapongeza sana wataalam wa ICT wa TMA kwa kufanya kazi zao kwa weledi. Alimalizia kwa kuipongeza menejiment nzima ya TMA kwa kazi nzuri inayofanyika.

“Nawapongeza sana kati ya taasisi za hali ya hewa ambazo kampuni yangu imekagua katika nchi mbali mbali duniani sijawahi kuona taasisi ambayo huduma zake zinaendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka kama ilivyo kwa TMA. Mwaka huu sina hoja yoyote mifumo yote imeboreshwa, wafanyakazi wana weledi wa hali ya juu na wanafahamu wanachokifanya, taratibu zote mlizojiwekea mnazitekeleza ikiwemo jinsi ya kutoa utabiri na kuufikisha kwa watumiaji katika sekta ya usafiri wa anga kwa wakati, utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa katika anga, uhakiki wa usahihi wa utabiri unaotolewa katika sekta ya usafiri wa anga, upimaji wa weledi wa watumishi wanaofanyakazi katika viwanja vya ndege, hali ilivyokuwa 2018 sivyo ilivyo 2019 uboreshaji ni wa hali ya juu, nawapongeza sana”. Alisema Bwana Frank kutoka kampuni ya Certech iliyoko nchini Canada.

Alhamisi, 22 Oktoba 2020

TMA IMETOA RASMI MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA ZA MSIMU MARA MOJA KWA MWAKA.



 

Dar es Salaam,Tarehe 21/10/2020:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ikijumuisha mikoa iliyopo magharibi mwa nchi ( Kigoma, Tabora na Katavi), nyanda za juu kusini magharibi (Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa), katikati mwa nchi (Dodoma na Singida), pwani ya kusini (Lindi na Mtwara), mkoa wa Ruvuma pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro na pia kuelezea athari zinazoweza kujitokeza. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika.  

‘Naendelea  kuwahimiza  wananchi waishio katika mikoa husika kuhifadhi mazao baada ya kuvuna kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam ili kuepuka uharibifu unaoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua na unyevunyevu inayotarajiwa kwani maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani’  alisema Dkt. Kijazi.

Kuhusu mvua za msimu wa Vuli kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ilielezwa kuwa zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo alisisitiza kuwa mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari 2020.

 

Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka utabiri ulionesha katika maeneo mengi ya  mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, Kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani huku mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi mvua zikitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

 

Dkt. Kijazi aliendelea kuelezea kuwa mvua hizo kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajiwa kuanzia mkoa wa Tabora katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 na baadae kutawanyika katika mikoa mingine ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 na ikitarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya nchi katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, japo kwa mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuisha katikati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021.


Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1603277722-NDJFMA_2020_21_SWA.pdf

Jumanne, 8 Septemba 2020

VULI: MAENEO MENGI YA NCHI YANATARAJIWA KUPATA MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI.




Wastani wa muda mrefu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Disemba

Dar es Salaam, 08/09/2020;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2020 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu  na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni  Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara  pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu).

 

Dkt Kijazi alisema, mvua za Vuli kwa mwaka huu zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, aidha mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, na ukanda wa pwani ya Kaskazini pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

 

Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema  upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji unatarajiwa.

 

“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo, nitoe angalizo,ingawaje maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani  hadi  wastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kijazi

 

Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2020 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu www.meteo.go.tz