![]() |
| Wastani
wa muda mrefu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Disemba |
Dar es Salaam, 08/09/2020;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2020 kwa maeneo yanayopata mvua mara
mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi
Mkuu na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara
mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa
ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha
kisiwa cha Mafia Tanga
na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa
ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu).
Dkt
Kijazi alisema, mvua za Vuli kwa mwaka huu zinatarajiwa
kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya
ukavu katika maeneo mengi ya nchi, aidha mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kwa
kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 katika maeneo
ya nyanda za juu kaskazini mashariki, na ukanda wa pwani ya Kaskazini pamoja na
kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.
Akizungumza kuhusu athari
zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa
kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji
safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo uwezekano
wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji unatarajiwa.
“Matukio
ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, mamlaka husika zinashauriwa
kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo, nitoe angalizo,ingawaje
maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi
wastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa
yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kijazi
Utabiri wa msimu wa mvua za
vuli 2020 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya
mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu
www.meteo.go.tz

