Alhamisi, 22 Oktoba 2020

TMA IMETOA RASMI MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA ZA MSIMU MARA MOJA KWA MWAKA.



 

Dar es Salaam,Tarehe 21/10/2020:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ikijumuisha mikoa iliyopo magharibi mwa nchi ( Kigoma, Tabora na Katavi), nyanda za juu kusini magharibi (Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa), katikati mwa nchi (Dodoma na Singida), pwani ya kusini (Lindi na Mtwara), mkoa wa Ruvuma pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro na pia kuelezea athari zinazoweza kujitokeza. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika.  

‘Naendelea  kuwahimiza  wananchi waishio katika mikoa husika kuhifadhi mazao baada ya kuvuna kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam ili kuepuka uharibifu unaoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua na unyevunyevu inayotarajiwa kwani maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani’  alisema Dkt. Kijazi.

Kuhusu mvua za msimu wa Vuli kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ilielezwa kuwa zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo alisisitiza kuwa mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari 2020.

 

Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka utabiri ulionesha katika maeneo mengi ya  mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, Kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani huku mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi mvua zikitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

 

Dkt. Kijazi aliendelea kuelezea kuwa mvua hizo kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajiwa kuanzia mkoa wa Tabora katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 na baadae kutawanyika katika mikoa mingine ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 na ikitarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya nchi katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, japo kwa mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuisha katikati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021.


Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1603277722-NDJFMA_2020_21_SWA.pdf

Jumanne, 8 Septemba 2020

VULI: MAENEO MENGI YA NCHI YANATARAJIWA KUPATA MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI.




Wastani wa muda mrefu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Disemba

Dar es Salaam, 08/09/2020;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2020 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu  na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni  Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara  pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu).

 

Dkt Kijazi alisema, mvua za Vuli kwa mwaka huu zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, aidha mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, na ukanda wa pwani ya Kaskazini pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

 

Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema  upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji unatarajiwa.

 

“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo, nitoe angalizo,ingawaje maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani  hadi  wastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kijazi

 

Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2020 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram. Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti yetu www.meteo.go.tz

 


Jumatano, 5 Agosti 2020

NANENANE 2020: WANANCHI WAMIMINIKA TMA NYAKABINDI.

Simiyu; Tarehe 04/08/2020

Wananchi mbalimbali katika mkoa wa Simiyu wametembelea banda la Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kupata elimu ya hali ya hewa inayotolewa na wataalam kutoka Mamlaka. Akizungumza wakati na wananchi hao kwa nyakati tofauti tofauti, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, alisema TMA ni taasisi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi hususan katika sekta zote za kiuchumi na kijamii. 

“Basi mwananchi tunakuomba utumie taarifa zetu za hali ya hewa ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zetu za kimaendeleo, na katika azma nzima ya kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda”. Alisema Dkt. Chang’a.

Aidha, aliendelea kusisitiza kuwa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ni chachu kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi, huku akisisitiza wananchi kuchagua vingozi bora kwa maendeleo ya nchi yetu ambayo tayari imefikia uchumi wa kati.

Kwa upande wa Meneja wa Kanda ya Ziwa-TMA, Ndg. Augustine Nduganda aliwakaribisha wananchi wa Kanda ya Ziwa hususan Mashariki, kutembelea banda la TMA ili waweze kupata elimu ya sayansi ya hali ya hewa kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kujionea vifaa vya hali ya hewa, jinsi uangazi, uchambuzi na utayarishaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwemo utabiri unavyofanyika na pia kupata elimu kuhusus mabadiliko ya hali ya hewa.








Jumanne, 9 Juni 2020

TANZANIA YAONGOZA MKUTANO WA KUWIANISHA SHUGHULI ZA UTOAJI HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA UKANDA WA SADC.



Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akiongoza Mkutano wa SADC Sekta ya Hali ya Hewa uliofanyika kwa njia ya mtandao katika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Jijini, Dar es Salaam. Aliyekaa kulia kwake ni Meneja Ushirikiano wa Hali ya Hewa Kimataifa wa TMA, Bw. Wibert Muruke akifuatilia majadiliano ya kikao

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akijibu hoja za wajumbe wa mkutano wa SADC Sekta ya Hali ya Hewa. Aliyekaa kulia kwake  ni Meneja Ushirikiano wa Hali ya Hewa Kimataifa wa TMA, Bw. Wibert Muruke akiandika muhtasari wa kikao

Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano wa kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC (Harmonizing SADC Strategy and Action Plan on Meteorology).

Mkutano huo ulifanyika tarehe 4 Juni 2020 kwa njia ya mtandao (videoconference) chini ya Uenyekiti wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambapo  Mkurugenzi Mkuu wa  TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliongoza mkutano huo.

Akiwasilisha hotuba yake fupi ya ufunguzi, Dkt. Kijazi alisema kuwa dhumuni kuu la mkutano huo ni kuwianisha shughuli  za  utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC ili zichangie ipasavyo katika kutatua changamoto za  sekta ya hali ya hewa katika Ukanda wa SADC kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Nchi Wanachama. Dkt. Kijazi alizitaja baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya hali ya hewa kuwa ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kupima hali ya hewa; kuchakata takwimu za hali ya hewa; na kubadilishana takwimu za hali ya hewa.

Dkt. Kijazi aliendelea kueleza kwamba, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Nchi Wanachama kuboresha huduma za hali ya hewa, utatuzi wa changamoto hizo unahitaji pia juhudi za pamoja za wadau na taasisi zote husika ili kuwianisha shughuli za huduma ya hali ya hewa za Kikanda.

 “Licha ya jitihada zilizofanywa na Nchi wanachama katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, bado kuna changamoto nyingi.  Kama sehemu ya utatuzi  wa changamoto hizi, mkutano huu utajadili namna ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa za Kikanda” alisema Dkt. Kijazi na kuwaomba wajumbe kushiriki kikamilifu na kutoa maoni  yatakayofanikisha  uwianishaji wa shughuli hizo.

Akitoa maelezo ya awali kuhusiana na mkutano huo, Afisa Mwandamizi wa Programu ya Hali ya Hewa katika Secretarieti ya SADC, Dkt. Prithiviraj Booneeady, alisema hatua ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ni takwa la  Itifaki ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) unaozitaka Nchi Wanachama kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa ili kuwezesha ushirikiano wa Kikanda na kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.  Kwa mujibu wa Dkt. Booneeady, hatua hiyo itasaidia juhudi za pamoja katika kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.

Mada zilizowasilisha katika mkutano huo ni pamoja na zinazohusiana na programu za Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) katika ukanda wa SADC; Programu za Secretarieti ya SADC zinazohusiana na sekta ya hali ya hewa;  Programu za Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Afrika (SADC MASA). Mkutano ulijadili shughuli hizo na kutoa mapendekezo. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kurejewa upya kwa Itifaki ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport, Communication and Meteorology) ili ukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya hali ya hewa.

Jumatatu, 23 Machi 2020

KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, DKT. AGNES KIJAZI ATOA WITO KWA WADAU WOTE WA HALI YA HEWA KUENDELEA KUZIELEWA NA KUTUMIA IPASAVYO TAARIFA ZA HALI YA HEWA ZITOLEWAZO NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA.

Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani (the World Meteorological Day-WMD), siku ambayo Jumuiya ya Hali ya Hewa duniani kote inaadhimisha kumbukizi la siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila Nchi mwanachama wa WMO na kuratibiwa na Taasisi za Hali ya Hewa za nchi husika. Taasisi hizo hutumia siku hii kuonyesha na kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa.
Kwa hapa nchini kwetu Tanzania, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). TMA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kabla ya hapo taasisi hii ilikuwa ni wakala wa serikali.
Katika kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”. Kaulimbiu hii inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji.
Kwa kawaida maji yapo katika hali mbalimbali ambazo ni yabisi (barafu), kimiminiko (maji ya kawaida) na gesi (mvuke). Hali hizo zinatokana na mzunguko ambao maji hupitia ujulikanao kama hydrological cycle unaohusisha ardhi, anga, bahari, maziwa, misitu na mazingira mengine. Ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari, mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso wa dunia. Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji. Changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kupelekea upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ni ongezeko la kina cha bahari Duniani kote. Hii husababishwa na mambo makubwa mawili: kwanza, ni kutanuka kwa maji ya bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji, na pili ni kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika. Ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo ili kuyafanya bora na yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.
Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo.
Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate sensitive sectors) ikiwemo sekta ya maji.
Katika kutimiza mahitaji ya wadau na matakwa ya program ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA, Mamlaka ya Hali ya Hewa hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali ya hewa. TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye uso wa dunia nchi kavu (ground weather stations), vilivyopo bandarini (marine weather stations) na vilivyopo katika anga la juu ambavyo vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations).
Aidha, TMA hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwaajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi. Utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast), mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, zikiwa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi hali ya hewa na maji. Aidha, TMA hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji. Utabiri huu husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS).
TMA imeendelea kupata mafanikio zaidi katika kutekeleza mpango mkakati wake. Mafanikio hayo ni pamoja na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Huduma Bora “Quality Management System (QMS) na kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.
Katika eneo la vifaa vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Mkakati huu umelenga kuboresha vituo vyote vya hali ya hewa nchini ili kuendana na ukuaji wa teknolojia ya hali ya hewa duniani, na pia kutekeleza mkataba wa Minamata (Minamata Convention) unaozitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kusitisha matumizi ya zebaki kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2020.
Hata hivyo pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji jitihada za wadau wote wa huduma za hali ya hewa, wakiwemo wadau wa maendeleo “Development Partners (DPs)” ili kuunga mkono na kuendeleza jitihada za Serikali. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za sekta maalumu na maeneo madogomadogo (downcaled information) na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.
Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani Kwa mwaka huu wa 2020, napenda kutoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka katika sekta zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Taifa letu. Napenda pia kuwaomba wadau wote kutuunga mkono katika utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS) ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini na kupunguza athari kwa jamii na sekta ambazo zinaathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo sekta ya maji.
Mwisho, nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD) 2020 yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”

MHE. MHANDISI ISACK KAMWELWE AONGEA KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 2020.

Kila mwaka tarehe 23 Machi, Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization-WMO) ambalo lilianzishwa tarehe 23 Machi, 1950. Tanzania pamoja na wanachama wengine 192 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani inaungana na jumuiya ya kimataifa kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii pia hutumika kuonesha mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za hali ya hewa ikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuchangia maendeleo na kukuza ustawi wa jamii. Taasisi za Hali ya Hewa duniani kote hutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa ambazo ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao.
Katika kusherehekea siku ya hali ya hewa duniani, ni desturi kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kutoa kaulimbiu ya maadhimisho ya kila mwaka. Kwa mwaka huu wa 2020 kaulimbiu ya maadhimisho haya ni “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water). Kaulimbiu hii inaelezea ukweli kwamba, hali ya hewa ina mchango mkubwa katika mtawanyiko, mgawanyo, ubora na matumizi ya rasilimali maji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile kilimo, nishati, mifugo na uvuvi. Pia kwa kuzingatia kuwa mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi pamoja na matukio ya hali mbaya ya hewa inayoambatana na mabadiliko hayo yanaathiri sana mzunguko wa maji wa Dunia pamoja na upatikanaji na ubora wa maji.
Kwa upande wa Tanzania, kama ilivyo kwa wanachama wengine wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ina jukumu la kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wa hali ya hewa ambao huchangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa rasilimali maji. Upatikanaji wa rasilimali maji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa na malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals-SDGs). Huduma za hali ya hewa ni muhimu katika malengo hayo hususani lengo Na. 7 (SDG7) ambalo linahusiana na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Tanzania inaendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoahuduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa. Hii ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalam ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwemo sekta ya maji. Mwaka 2019, Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya
2019. Sheria hii inaiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Pia sheria iliyounda Mamlaka ya Hali ya Hewa inaipa nguvu za kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Aidha, Sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo sheria hii imehakikisha uwakilishi, ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za kijamii.
Katika kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini, Serikali inaendelea kuijengea uwezo Mamlaka hii ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mfupi na muda mrefu (climate variability and change). Taarifa za hali ya hewa ni za muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Taarifa na huduma za hali ya hewa husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu na hivyo kuliandaa taifa vizuri katika kukabiliana na maafa yanayosababishwa na vipindi vya ongezeko au upungufu wa maji kama vile mafuriko na ukame. Mfano wa uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko ni pamoja na mvua kubwa zilizonyesha katika msimu huu na kuharibu miundominu ya usafiri ikiwemo miundombinu ya reli, barabara na madaraja. Hivyo, huduma za hali ya hewa zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo, maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati, ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli yakiwemo madaraja na uratibu wa maafa miongoni mwa sekta nyingine. Aidha, katika jitihada za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa TMA kwa kuboresha mtandao wa Taifa wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa data na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango ya maendeleo katika sekta hizo.
Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa, Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini. Kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Juamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo imeboresha utendaji wa TMA katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hatuna budi kutumia huduma hizi ili kuboresha shughuli zetu za kila siku na vilevile kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuboresha huduma hizi kwa siku zijazo.
Uwekezaji wa Serikali katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hususani katika kuboresha miundombinu ni pamoja na ununuzi wa Rada za hali ya hewa kwa lengo hilo hilo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Rada hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya ununuzi ambazo zitafungwaMtwara, Mbeya na Kigoma. Aidha, ili kukamilisha mtandao wa Rada zitahitajika Rada zingine mbili ambazo zitafungwa Dodoma na Kilimanjaro. Pia kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa huduma za hali ya hewa na changamoto zinazotukabili ambazo zinahitaji kutatuliwa, Serikali itaendelea kuwekeza ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa wataalamu na miundombinu huku tukihimiza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali zinazohusiana na zinazotumia huduma za hali ya hewa na rasilimali maji kwa lengo la kuendelea kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Vilevile kwa kuzingatia maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini, ni vyema kuongeza juhudi katika kutumia huduma hizi katika mipango ya sekta zote za kiuchumi na kijamii na utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji.
Katika kuadhimisha Siku hii ya hali ya hewa Duniani yenye kauli mbiu “Hali ya Hewa na Maji” (Climate and Water), ninatoa wito kwa wadau wote wa huduma za hali ya hewa kutoka sekta zote za kiuchumi na kijamii zinazotumia au kuathiriwa na hali ya hewa pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanazitumia huduma za hali ya Hewa kwa maendeleo ya Taifa letu. Sekta ya maji izitumie huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango yao ili kwenda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu. Aidha, tuendelee kuunga mkono juhudi za TMA katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na udhibiti kwa kuendelea kuwapa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wote wenye vituo vya hali ya hewa wanavinasajili TMA ili kwenda sambamba na matakwa ya sheria. Ushirikiano huo utaiwezesha TMA kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa hapa nchini.
Mwisho nachukua fursa hii kuwatakia wananchi wote pamoja na jumuia yote ya kimataifa maadhimisho mema na yenye mafanikio ya siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2020.