![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu
wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi akijibu hoja za wajumbe wa mkutano wa SADC
Sekta ya Hali ya Hewa. Aliyekaa kulia kwake
ni Meneja Ushirikiano wa Hali ya Hewa Kimataifa wa TMA, Bw. Wibert
Muruke akiandika muhtasari wa kikao
Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano wa kuwianisha shughuli
za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika Ukanda wa SADC (Harmonizing SADC
Strategy and Action Plan on Meteorology).
Mkutano huo ulifanyika tarehe 4 Juni 2020 kwa njia ya mtandao
(videoconference) chini ya Uenyekiti wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA), ambapo Mkurugenzi
Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi aliongoza mkutano huo.
Akiwasilisha
hotuba yake fupi ya ufunguzi, Dkt. Kijazi alisema kuwa dhumuni kuu la mkutano huo
ni kuwianisha shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa katika
Ukanda wa SADC ili zichangie ipasavyo katika kutatua changamoto za sekta ya hali ya hewa katika Ukanda wa SADC
kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika Nchi Wanachama. Dkt.
Kijazi alizitaja baadhi ya changamoto zinazokabili sekta ya hali ya hewa kuwa
ni pamoja na uhaba wa miundombinu ya kupima hali ya hewa; kuchakata takwimu za
hali ya hewa; na kubadilishana takwimu za hali ya hewa.
Dkt.
Kijazi aliendelea kueleza kwamba, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Nchi
Wanachama kuboresha huduma za hali ya hewa, utatuzi wa changamoto hizo
unahitaji pia juhudi za pamoja za wadau na taasisi zote husika ili kuwianisha
shughuli za huduma ya hali ya hewa za Kikanda.
“Licha ya jitihada zilizofanywa na
Nchi wanachama katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, bado kuna
changamoto nyingi. Kama sehemu ya
utatuzi wa changamoto hizi, mkutano huu
utajadili namna ya kuwianisha shughuli za huduma za hali ya hewa za Kikanda”
alisema Dkt. Kijazi na kuwaomba wajumbe kushiriki kikamilifu na kutoa
maoni yatakayofanikisha uwianishaji wa shughuli hizo.
Akitoa
maelezo ya awali kuhusiana na mkutano huo, Afisa Mwandamizi wa Programu ya Hali
ya Hewa katika Secretarieti ya SADC, Dkt. Prithiviraj Booneeady, alisema hatua ya kuwianisha shughuli za
huduma za hali ya hewa ni takwa la Itifaki
ya SADC ya Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport,
Communication and Meteorology) unaozitaka Nchi Wanachama kuwianisha shughuli za
huduma za hali ya hewa ili kuwezesha ushirikiano wa Kikanda na kuimarisha uwezo
wa Nchi Wanachama katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Kwa mujibu wa Dkt. Booneeady, hatua hiyo
itasaidia juhudi za pamoja katika kuimarisha uwezo wa Nchi Wanachama katika
kukabiliana na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.
Mada
zilizowasilisha katika mkutano huo ni pamoja na zinazohusiana na programu za Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO) katika ukanda wa SADC; Programu za Secretarieti
ya SADC zinazohusiana na sekta ya hali ya hewa; Programu za Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa
Kusini mwa Afrika (SADC MASA). Mkutano ulijadili shughuli hizo na kutoa
mapendekezo. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kurejewa upya kwa Itifaki ya
Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (SADC Protocol on Transport,
Communication and Meteorology) ili ukidhi mahitaji ya sasa ya sekta ya hali ya
hewa.

