Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kumiliki
cheti cha kimataifa cha uthibitisho wa utoaji huduma bora za hali ya hewa
katika sekta ya usafiri wa anga kwa mara nyingine. Mamlaka ambayo imekuwa na
cheti hiki kwa miaka kumi sasa, ni miongoni mwa Taasisi chache za hali ya hewa barani
Afrika kufanikiwa kushikilia cheti hicho kwa kipindi kirefu.
Mafanikio hayo yamepatikana
baada ya kukamilika kwa ukaguzi uliofanyika kwa njia ya mtandao na
Kampuni ya Kimataifa ya Certech kutoka Canada, kuanzia Tarehe 11 hadi 15
Januari 2021 katika vitengo na ofisi mbalimbali ndani ya Mamlaka, Makao Makuu
na Mikoani. Ukaguzi huu ulifanyika kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyowekwa
na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO 9001:2015) na ulimalizika kwa taarifa
nzuri ya kwamba TMA imeboresha sana mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo
inastahili kuendelea kumiliki cheti hicho cha ubora cha kimataifa.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt.
Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO), alisema kuwa Mamlaka imeanza kumiliki cheti hicho cha ubora
tangu mwaka 2011, ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa Taasisi za Hali ya
Hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho kwa vigezo vya ubora
vilivyoainishwa katika mwongozo wa “ISO 9001:2008”, na ilipofika mwaka 2017
Tanzania kupitia TMA ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha inafanikiwa kupata
cheti kipya kwa mujibu wa vigezo vipya vya “ISO 9001:2015,” ambacho kiliifanya Tanzania
kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa nchi ya tatu barani Afrika ambayo taasisi yake
ya hali ya hewa imepata cheti hicho kabla ya Septemba 2018 iliyokuwa ni mwisho wa matumizi ya cheti cha
zamani.
“Mamlaka imekuwa ikikaguliwa kimataifa kila mwaka na mkaguzi
kutoka nje ya nchi ili kuangalia ubora wa huduma zitolewazo, ni furaha kubwa
kuona bado TMA inaendelea kuwa taasisi ya mfano kwa taasisi zingine za hali ya
hewa barani Afrika na nje ya Afrika kwa kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa.
Mpaka sasa TMA imefanikiwa kutoa mafunzo kwa baadhi ya taasisi za hali ya hewa
katika nchi za SADC, EAC na zingine zikiwemo
Saudi Arabia, Libya, Nigeria, Maldives, n.k kuhusu jinsi ya kufanikisha upatikanaji
wa cheti hiki pamoja na kuboresha weledi wa wataalamu katika Taasisi zao za Hali
ya Hewa. Mafanikio haya ni kutokana na ‘team work’ iliyopo baina ya menejimenti
na watumishi wa Mamlaka, weledi, bidii na miongozo mizuri tuliyojiwekea ya kuhakikisha
tunafanikiwa ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa ukaguzi wa ndani mara kwa mara”.
Alisema Dkt. Kijazi.
Aliongeza kwa kusema kwamba upatikanaji wa cheti hicho
unaihakikishia dunia kwamba anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa
liko salama kwa ndege zote za kimataifa kuruka kwani ilishakubalika kimataifa
kwamba kwa nchi ambazo taasisi zao za hali ya hewa hazijapata cheti hicho cha
ubora ndege hazitaruka katika anga la nchi hizo. Dkt. Kijazi alisema TMA
inajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia sekta
ya usafiri wa anga kwani katika viwanja vyote vya ndege nchini huduma za hali
ya hewa zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Hata katika viwanja
ambavyo ndege hazitui kwa saa 24, TMA inaendelea kupima hali ya hewa katika
viwanja hivyo kwa saa 24 ili kukidhi matakwa ya kimataifa katika utoaji wa
huduma za hali ya hewa. Aliwapongeza watumishi wa TMA kwa kazi kubwa
wanayoifanya kuhakikisha TMA inatimiza majukumu yake.
Awali wakati akikamilisha ukaguzi huo, mkaguzi wa nje kutoka
Certech - Canada Bwana Frank Strohmeier, alisema TMA imekuwa ikiboresha kila
mara mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo kwa mwaka huu, hapakuwa na hoja (nonconformity)
yoyote ambayo ingehitaji kutolewa maelezo na kupelekea kuhitajika kwa marekebisho
katika mfumo wa utoaji huduma. Hivyo maeneo yote ambayo TMA imekaguliwa
yamekuwa na ubora wa hali ya juu pasipo kuwa na mapungufu yoyote. Alifurahishwa
na jinsi ambavyo ukaguzi umefanyika kwa njia ya mtandao ukiwa na mafanikio
makubwa pasipo changamoto yoyote ya teknolojia hivyo akawapongeza sana wataalam
wa ICT wa TMA kwa kufanya kazi zao kwa weledi. Alimalizia kwa kuipongeza
menejiment nzima ya TMA kwa kazi nzuri inayofanyika.
“Nawapongeza sana kati ya taasisi za hali ya hewa ambazo
kampuni yangu imekagua katika nchi mbali mbali duniani sijawahi kuona taasisi
ambayo huduma zake zinaendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka kama ilivyo kwa TMA.
Mwaka huu sina hoja yoyote mifumo yote imeboreshwa, wafanyakazi wana weledi wa
hali ya juu na wanafahamu wanachokifanya, taratibu zote mlizojiwekea
mnazitekeleza ikiwemo jinsi ya kutoa utabiri na kuufikisha kwa watumiaji katika
sekta ya usafiri wa anga kwa wakati, utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa
katika anga, uhakiki wa usahihi wa utabiri unaotolewa katika sekta ya usafiri
wa anga, upimaji wa weledi wa watumishi wanaofanyakazi katika viwanja vya ndege,
hali ilivyokuwa 2018 sivyo ilivyo 2019 uboreshaji ni wa hali ya juu, nawapongeza
sana”. Alisema Bwana Frank kutoka kampuni ya Certech iliyoko nchini Canada.
